Viwanja vya Bunge mjini Dodoma vimetawaliwa na Vazi la Kijani leo baada ya zaidi ya Wabunge 200 wa Chama cha Mapinduzi CCM kukusanyika pamoja kwa ajili ya uchaguzi wa Mgombea wa Uspika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Siku ya Alhamisi Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi ilikutana katika Makao Makuu ya Chama hicho na kuyachuja Majina ya Wagombea 15 waliokuwa wameomba ridhaa hiyo. Jukumu la Kamati hiyo lilikuwa ni kubakiza Majina Matatu tu na ndipo:
Mama ANNA MAKINDA.....
Mama Makinda akiomba kura kutoka kwa Mmoja wa wajumbe wa Mkutano wa Kamati ya Wabunge wa CCM.
Mama ANNA ABDALAH.....
Hapo Mama Abdalah mwenye Kijani akiomba kura kutoka kwa Mama Sophia Simba muda mfupi kabla kuanza kwa uchaguzi.
Na Mama KATE KAMBA....
Mama Kamba akiomba kura kutoka kwa Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.
Basi hao ndio Wagombea Watatu waliopita katika mchujo huo wa NEC. Wote watatu ni Wanawake. Kwa nini?
Katibu wa CCM Yusuf Makamba anasema kuwa ni mpango wa makusudi wa chama chao ukilenga kuchochea zaidi vuguvugu la harakati za kumkomboa Mwanamke. Wanaamini kwa kufanya hivyo, mgombea atakayepita basi atakiwakilisha chama vizuri katika kinyang'anyiro cha Uspika na hatimaye Bunge hilo kupata kiongozi wake mkuu ambaye ni Mwanamke.
Tangu Tanzania imepata uhuru haijawahi kuwa na kiongozi mkuu mwanamke katika mihili yake yote mitatu ya nchi. Na Makamba anasema wamedhamiria kuifuta rekodi hiyo nchini na hatimaye kuandika historia mpya kwa moja ya mihili mitatu ya Taifa kuongozwa na Mwanamke. Ni mpango mzuri kwa kweli unaolenga kumkweza Mwanamke MWENYE UWEZO WA KUONGOZA. Mpango huo utawezekana? Tusubiri tuone.
Rungu la Kamati ya Wabunge wa CCM limekaa pia na kupiga kura za maoni za kumchagua mgombea mmoja kati ya hao Watatu. Na baada ya uchaguzi huo, taarifa iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa CCM Kepteni John Chiligati ni kuwa Mheshimiwa ANNA MAKINDA ndiye mgombea wa uspika wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mama Makinda amepata kura 211 kati ya 241 zilizopigwa. Mama Abdalah amepata kura 14 wakati Mama Kamba amepata kura 15, huku kura Moja tu ikiharibika.
Je, enzi za 'zama za spidi na viwango ndio zimeisha?'
"...amani ya ndani ya Bunge ni kanuni...," ni kati ya kauli alizozitoa Mama Makinda kuhusiana na utendaji wake wa kazi bungeni endapo atapata nafasi ya kuiongoza taasisi hiyo. Anasema kila jambo lina taratibu zake na hivyo kila Mbunge anapaswa kuzielewa kwa umakini kanuni zinazoliongoza Bunge ili awe na mahusiano mazuri na kiti cha Spika na akimalizia, "....ni kama mpira wa Miguu, lazima ucheze kwa kufuata sheria...."
Furaha kama hiyo itadumu endapo Mama Makinda atashinda uchaguzi wa Spika. Katika kinyang'anyiro hicho anakumbana na Wakili MABERE MARANDO ambaye amepitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA. Wabunge kwa umoja wao wataamua wanamuhitaji nani kati ya hao Wawili ili awe Spika wao mpya.
Ikumbukwe kuwa, hili ni Bunge lililotokana na hamasa ya Siasa waliyonayo Watanzania kwa hivi sasa. Ni hamasa hiyo iliyopelekea Bunge la Kumi kuongeza Wabunge wa kambi ya Upinzani....kuongeza kundi la Vijana kutoka Vyama vyote....kuongeza kundi la Wasomi......na hata viongozi wa dini.
Spika ajae ni vyema akaliangalia ongezeko la makundi hayo na kujua namna ya kufanya nayo kazi kwa pamoja bila mikwaruzano ya hapa na pale hisiyo na msingi kwa maendeleo ya Mtanzania.
Kila la kheri Mama Anna Makinda.....
No comments:
Post a Comment