Friday, May 14, 2010

HARAKATI ZA VIJANA WA KIBONGO KUCHUMIA JUANI

Je unakumbuka?Mwaka 2005 wakati Rais Ja kaya Mrisho Kikwete akijinadi kwa Watanzania ili aweze kupata nafasi aliyonayo sasa, aliwaahidi Wabongo kuwa ataongeza ajira kwa vijana......vijana hawa unaowajua ambao kwa asilimia kubwa wanalijaza Taifa.

Hoja ni je, ahadi ya Mheshimiwa JK inatekelezeka? Wakati baadhi yetu tukiendelea kuwa na Swali kama hilo vichwani mwetu, baadhi ya wakosoaji wa ahadi hiyo wanasema kuwa hali imeonekana kuwa bado si nzuri kutokana na vijana wengi kukosa ajira. Na Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2009 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mamilioni ya vijana nchini wameendelea kukosa kazi ama ajira rasmi.

"NASAKA BIDHAA LAKINI SOKO JE.....!!!!!

Baadhi ya Vijana hawapo nyuma katika utafutaji na kila kukicha wanasaka shughuli mbalimbali za uzalishaji ili waweze kujikimu na maisha yao. Kijana kama huyo hapo juu angalau ana mahali pa kuingizia riziki lakini uhakika wa soko la kazi yake upo vipi?

Kizazi kichanga kama hiki kinapojibiidisha kwa nguvu zote na kukosa masoko ya bibdhaa zao inamaanisha nini? Kwa mtindo huo tunawezaje kuwaaminisha kuwa shughuli zao zitawawezesha kupiga vita umasikini? Naamini Masoko ya uhakika kwa ajili ya shughuli zao itakuwa ni kichocheo maridhawa kinakachomhamasisha kijana kujishughulisha kwa bidii na kuondokana na umaskini.

Nikirejea tena katika utafiti wa LHRC, wanasema kuwa zaidi ya Watanzania milioni 2.3 kwa upande wa Tanzania Bara wanafanya kazi zisizo rasmi. Na wengi wa wafanyakazi hao ni vijana ambao wanafanya kazi ndogo ndogo maarufu kama ‘machinga.’ Dar es Salaam peke yake inakadiriwa kuwa na zaidi ya vijana milioni 1.6 ambao hawana ajira ya uhakika.

SHUBIRI YA JUA KALI LA SEKTA ZISIZO RASMI!!!!!!

Masikini Kijana kama huyo 'Machinga' wa mjini Dodoma baada ya kuzunguka sana juani bila kupata chochote, ona sasa ameuchapa Usingizi hadharani pasipo mapenzi yake. Biashara anayofanya ni ya kuuza visu. Na hapo akinogewa na usingizi tu anaviangukia visu vyake ambavyo ameviweka kwenye Meza!!!!!!

Moja ya mambo yanayotajwa kama kichocheo cha Vijana wengi kukosa ajira ni ukosefu wa mfumo mzuri wa elimu. Hali hiyo inasababisha vijana wengi kushindwa kupata ajira pindi wamalizapo shule kutokana na kukosa elimu ya vitendo kwani nadharia imechukua nafasi kubwa mashuleni ikiwa hali hiyo haiendani na kabisa na mazingira halisi ya ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia.

FANYA KAZI KAMA MTUMWA HATA KAMA HAZINA MALENGO!!!!!!
Kijana kama huyo licha ya kuwa anawaburudisha watu wengi hapo ambao wanamtazama, kwa mtazamao wangu siwezi kuamini kuwa anafanya kazi yenye malengo kwa maisha yake ya baadae. Jasho linamtiririka kweli lakini mwisho wa siku anabaki na nini cha kumnufaisha zaidi ya kupewa sifa za kijinga tu kuwa "haaaaaa! Yule Mshikaji anakata mauno!!!!!!"

Sina mengi ya kusema. Mara nyingine napata wasiwasi kuwa hata sauti yangu itakauka wakati sina uhakika kama wawakilishi wa vijana huko Serikalini wanafikwa na maneno ama manunguniko kama haya! Lakini kwa kuwa ni muhimu kusema na nina uhuru wa kuelezea hisia zangu, basi.........

Serikali iendelee kuweka nguvu zaidi kwenye kuongeza ajira kwa vijana wenye sifa ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza kitaaluma ili waweze kutoa mchango mkubwa kwa taifa lao ambalo linawategemea kwani wao ndio nguvu kazi. Uwekezaji 'unaowezekana' kama wa kutengeneza dawa za kienyeji, ukulima wa matunda na nyingine nyingi waachiwe vijana na wazawa. Vijana waelimishwe juu ya mambo yanayowahusu kama vile kujua sera za maendeleo zinazowahusu wao.

VIJANA SI TAIFA LA KESHO. VIJANA NI TAIFA LA LEO.

Thursday, May 13, 2010

IDODOMYAAAAAAAAAAAAAAA

Mara ya mwisho kutoka nje ya kituo changu cha kazi ilikuwa ni hivi karibuni nilipotoka Mwanza na kwenda bungeni mjini Dodoma katika mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHESHIMIWA SPIIIIKAAAAAAAAAAAAAAAAAAA

Huo mjengo unavutia sana jamani. Na pia umepambwa na mandhari nyingi ambazo zinavutia pia kuanzia nje mpaka ndani ya mjengo huo.
MAJI YANAVYOJIACHIA SASA

Zipo sehemu nyingi tu zinazovutia kwa nje......sehemu nyingine nliyokuwa naipenda sana na ambayo nilikuwa naitumia kila siku ni hii hapa....

Hiyo ni kati ya njia za kuingia mjengoni. Njia hiyo ndio maalumu kwa Waandishi wa Habari kwani wametengewa hapo kwa ajili ya kuingilia mjengoni. Njia imerembwa kwa Maua mazuri kuliko njia zote bungeni.
SEHEMU YA NDANI

Mbali mjengo kuna vitu vingine ambavyo sitavisahau. Kwanza kwa ndugu zetu katika fani ya Habari. Jamani TBC Redio walikuwa na vifaa ambavyo kwenye Redio za FM ni nadra sana kuvikuta.

Naamini wengi wa Waandishi wa KIZAZI KIPYA wamekuwa wanaviona kwenye Picha tu vifaa kama hivyo wakati wa mafunzo yao. Wengi wetu tunarekodi mambo yetu kwa Digitali wakati wakongwe hao bado wanajivunia teknolojia ya Analojia. Nimeipenda sana hiyo.

Ngoja niwape shavu na wenzangu ambao tulikuwa wote mjengoni kikazi.
SALIM MLEGE A.K.A PROF katulia sana kwenye mambo ya Picha


MANGI MANYANGA alitusafirisha salama.


NYANDA NYANDA alihakikisha muonekano wa Picha unakuwa safi hewani


KAYENZE IBRAHIM (mwenye Laptop) alihakikisha Mitambo yote ipo katika usalama wake.


TOM CHILALA tumesaidiana sana kuandaa TUONGEE ASUBUHI na kuendesha BUNGE


RAFIKI ZETU MR. KANIKI na HENRY MABUMO walikuwa wanaiwakilisha ITV


RAFIKI mwiningine ni KURINGE MONGI wa CHANNEL TEN


Lakini moja siku ambazo sitazisahau katika kipindi hicho cha uzoefu wa bungeni ni siku ambayo.......
HUTUWEZI WEEWE...

Wabunge wanaotoka katika jamii za Wafugaji walipomjia juu Dokta Magufuli na miswada yake ya sekta ya Mifugo. Hapo unapowaona ni muda mfupi tu baada ya Waziri Magufuli kutangaza kuirudisha Miswaada hiyo kwenye Kamati ili ikajadiliwe upya.
Na baada ya ushauri wao pamoja na wana Kamati, mwishoni mwa Bunge Miswaada hiyo ilirejeshwa na ikapita. Ni tukio ambalo nilimuona Magufuli anarudi nyuma na kujilpanga upya tofauti na ilivyozooleka harakati zake huwa zikianza zinasonga mpaka ukomo wake.
Kwa kweli hayo ni kati ya mambo ambayo nabaki nayo katika kipindi hicho nilichokuwa Dodoma....ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuingia bungeni na lilikuwa ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa 19. Kwa taarifa yako ni kuwa, uhai wa Bunge huwa unakamilishwa kwa Mikutano 20 kila baada ya uchaguzi Mkuu.

MERCI BEAUCOUP.

UTAFUTAJI RIZIKI NA MBINU ZAKE

Vijana wengi wanajishughulisha na mambo mbalimbali ya kujiingizia kipato. Na katika kutafuta kwao riziki basi wanakuwa na mbinu mbalimbali za kuwavutia wale wanaotaka kuwahudumia.

Hapa tunakutana na Kijana Mmoja ambaye amependeza sana kwa mwonekano wake. Lakini sasa biashara anayofanya nadhani hata na Wewe unaweza kustaajabu. Niskutamanishe saaaaaaaaaaaaaana, naomba nikukutanishe na Mdau BYABATO kwenye Kichwa cha Habari cha BIASHARA YA KAHAWA

Friday, May 7, 2010

MAJANGA YA MOTO NA SHUBIRI ZAKE

”Egraaa, utini weeeena……” haa haa haaa. Jamani ni salamu tu hiyo ya kisauzi sauzi; ni kama ‘habari yako’ kwa Kiswahili. Mambo ya kuelekea Kombe la Dunia 2010 katika ardhi ya Madiba.

Nakualika katika ukurasa huu ikiwa leo nina ajenda ya suala zima la kukabiliana na matukio ya Moto. Mara kadhaa katika jamii zetu hizi tumekuwa tukisikia matukio mbalimbali ya Moto yakitokea, na kwa matukio hayo wapo ambao wamepata majeraha makubwa na pengine ulemavu wa maisha.

Na wapo ambao wamepoteza maisha baada ya kukumbana na mikasa mbalimbali ambayo inatokana na majanga ya Moto. Jamani moto……moto….moto…..motoooooooo!



Kikubwa kinachoonekana baada ya majanga hayo kutokea ni changamoto ya kuukabili moto. Namaanisha kuwa wengi wetu bado hatujawa na uelewa ama mbinu za kupambana na majanga hayo…..matokeo yake huwa tunachanganyikiwa mapema na kushindwa pa kuanzia pindi tu moto unapowaka.



Tumewahi shuhudia pia matukio hayo yakisababisha watu kupoteza mali zao nyingi sana; wapo ambao wameangukia katika umasikini na mifano halisi ni maeneo ya biashara mathalani soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya pamoja na jengo la ushirika jijini Dar es Salaam ambapo majanga hayo yamewafanya wafanyabiashara kuwa masikini.

Historia ya Majanga ya Moto inaziangukia pia Shule mbalimbali za hapa nchini hususani Shule za Bwezi za Sekondari; Miongoni mwa matukio hayo ni lile la mwaka 1994 mkoani Kilimanjaro katika shule ya Sekondari Shauritanga ambapo zaidi ya wanafunzi Arobaini walipoteza maisha. Pia mwaka 2009 mkoani Iringa katika shule ya Sekondari Idodi, zaidi ya wanafunzi Kumi walipoteza maisha huku wengine zaidi ya Ishirini wakijeruhiwa vibaya na janga la moto.

JAMANI JAMANI!!!!

Wananchi wakishuhudia Miili ya baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Idodi mkoani Iringa.

INAUMA!

Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi Mheshimiwa Mwantumu Mahiza akilia kwa uchungu baada ya kushudia Mabinti wa Idodi waliteketea kwa janga la Moto.

Mungu azilaze roho za marehemu wote waliopoteza maisha kwa vifo vya namna hiyo ambavyo naamini ni kati ya vifo vya mateso sana katika dunia hii. Inauma.

Hivi karibuni jijini Mwanza, Kikosi cha Zimamoto na uokoaji cha jijini humo kimeanza mkakati mwingine wa utoaji mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto kwa wanafunzi wa Shule za msingi na Sekondari.

Bila shaka huu ni mpango mbadala na kwa kweli ni tofauti na ilivyozoeleka hapo awali kwa vikosi hivyo hapa nchini kutoa mafunzo ya namna hiyo kwenye viwanda, mashirika ya umma na binafsi pamoja na karakana mbalimbali…..lakini safari hii wamehamia kwa wanafunzi.

TWENDE KAZI SASA....MAFUNZO KWA VITENDO!!!!

Afisa wa Zimamoto jijini Mwanza Bwana Masood Gadafi akiwasha moto ikiwa ni ishara ya kuanza mafunzo.

Kwa kuzingatia msemo wa Wahenga wa Kale kwamba “Mtoto mkunje angali mbichi,” mafunzo hayo yamewalenga zaidi Wanafunzi lakini pia Walimu wao hawakuwekwa kando. Na lengo kuu hapa ni kuhakikisha kuwa watu wanakuwa na ujasiri wa kuwahi kuuzima moto mapema kabla haujasambaa.

Mbinu ya kwanza ni kuuzima moto kwa kutumia Blanketi maalumu (sasa kama hauna hilo Blanketi maalumu inakuaje?)

MWENDO WA KINYONGA NA UOGA JUU!!!!

Mwalimu Patrick Leonidas wa Shule ya Msingi Igoma akiwa na Blanketi maalumu tayari kuukabili moto unaoanza kuwaka.

Sasa Wataalamu wa Zimamoto wanasema kuwa kama hauna Blanketi hilo maalumu, unachofanya ni kutumia Blanketi lako la kawaida la kujifunika wakati wa baridi au unatafuta nguo ambayo unaamini ni kati ya nguo nzito ulizonazo….halafu hiyo nguo nzito ama Blanketi unalilowesha na Maji mengi kisha unaweza kuuzima Moto huo kabla haujasambaa.

“Heeeeeee Mwalimu wetu muogaaaaaa!”

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Igoma wakimshangilia Mwalimu wao Fatuma Mrumbi wakati akiukabili Moto.

Wataalamu wanasema ukishaweza kuubeba ujasiri wa kuufunika Moto huo kwa Blanketi, basi unakuwa umeweza kuepusha ile hali ya hewa kusambaa na kuufanya moto huo kuleta madhara na uharibifu mkubwa.



Mbinu nyingine ni ya kuzima Moto kwa kutumia gesi. Na mbinu zote hizo mbili ni lazima mzimaji akae upande ambao upepo unatoka.

Wanafunzi na Walimu wa Shule ya Msingi Igoma jijini Mwanza wakifuatilia kwa makini zoezi la kukabiliana na Moto unaoanza kuwaka.



Fikra zangu zinanishawishi kuamini kuwa Kikosi cha Zimamoto na uokoaji jijini Mwanza kimepiga hatua kwa kufikiria na kuamua kufikisha elimu hiyo kwa Wanafunzi wa shule ya msingi. Wanasaikolojia wanaamini kuwa Watoto wana uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo.

Kwa mujibu wa Bwana Julius Bulambu ambaye ni Mkuu wa kikosi hicho jijini Mwanza, wamechukua hatua hiyo kutokana na uzoefu walioupata kutoka katika baadhi ya nchi zilizoendelea kama vile Finland ambayo imepiga hatua ya kupambana na majanga ya moto kwa kufikisha mafunzo ya namna hiyo mara kwa mara kwa Wanafunzi.



Pengine kitu kingine cha msingi nachokiona ni kuwa shabaha ya kuwalenga watoto inaweza kuleta mabadiliko katika jamii…..na pengine taifa hilo la leo linaweza kuwa chachu nzuri ya kueneza elimu hiyo kwa jamii kulingana na walichojifunza.

Na endapo Wizara ya Elimu italiona hili, basi itakuwa ni vyema na kupendeza ikiwa Wizara hiyo itafikiria kuifanya elimu ya majanga ya moto kuwa ni sehemu ya mtaala katika masomo ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari hapa nchini.

Ninathubutu kuyanena hayo kwa kuwa ninaona wazi mpango huo utaisaidia jamii kupambana na Moto katika hatua za awali kabla ya Zimamoto hawajafika katika eneo la tukio. Sio kila siku tukae tunawasubiri kwa muda mreeefu wafike ili hali tukijua wazi kuwa Kikosi hicho bado hakijawa na uwezo wa kutosha.

Kazi kwenu na kila la kheri Zimamoto jijini Mwanza katika mpango wenu kufikisha elimu hiyo kwenye mikusanyiko ya watu wengi kama vile kwenye masoko na vituo vikuu vya usafirishaji wa abiria.

Wabilah Tawfiq. Aslaaam Aleikum.

Monday, May 3, 2010

USAFIRI WA BODABODA

HII NDO HALI HALISI YA USAFIRI WA BODABODA....KUKUTA DEREVA NA ABIRIA WAKE WOTE HAWAJAVAA KOFIA.

Na cha ajabu unakuta watu hao wanakatiza hata mbele ya Askari wa Usalama barabarani bila hata kuchukuliwa hatua. Ni hali halisi hiyo!!!!

LAKINI WAPO WANAOJALI KAMA HAWA NIMEWASHUHUDIA MITAA FULANI YA MWANZA.

Ila utamaduni huo wa Dereva na Abiria kuvaa Kofia ni nadra sana. Hata hao nilipowaangalia vizuri nikagundua kumbe ni Mafundi wa Cable TV wala si biashara ya Usafiri wa Abiria.

"ELIMU YA USAFI MASHIKOLO MAGENI?"

U bukheri jamani Msomaji wangu wa Ukurasa huu? Habari za siku nyingi. Mimi nafurahi na ninaona jinsi gani ilivyo vyema na kupendeza ambapo Mimi na Wewe tunakutana tena, tunakaa pamoja kwa umoja kuelezana mambo kadha wa kadha.

Jamani mara nyingi tumekuwa tukisikia harakati mbalimbali za kupambana na magonjwa ya milipuko mathalani Kipindupindu ambacho kila Mwaka kinakuja, watu wanalazwa kwa sana tu, wengine wanapoteza maisha; na kwa kuwa ni Ugonjwa wa msimu, basi inafikia hatua unatoweka na maisha yanaendelea kama kawaida.

Wapo wanaowanyooshea vidole Maafisa ama Mabwana na Mabibi afya wetu kuwa wanazembea sana katika suala la kuhamasisha Usafi. Kwa namna fulani ukweli inawezekana upo hapo; wala sibishani na huo mtazamo.

Tuuangalie upande wa pili. Hapa najitazama Mimi binafsi; jitazame na Wewe tukiwa wadau muhimu wa suala la Usafi. Nakualika hapa......



Hivi hao jamaa wote hawajui umuhimu wa kuwa wasafi? Hawajui umuhimu wa kuishi kwenye Mazingira ya usafi? Hawajui kuwa eneo kama hilo ni hatari kwa afya zao? Kisingizio cha ukata wa maisha kinaweza kuwa sababu ya kukubaliana na hiyo Picha?

Ninachotaka kusema ni kuwa.....Usafi ni suala la Mtu binafsi; wala haliitaji nguvu kutoka kwa Mtu mwingine eti aje akuhamasishe uwe msafi. Tuchukue tu mfano mdogo wa maisha yetu ya kila siku. Jiulize ni mara ngapi unanawa Mikono yako punde tu unapotoka Chooni!! Haijalishi umetoka kupata haja ndogo ama kubwa!!!????

Kwa mtindo huo wala hatuitaji kuwalaumu hao wenye dhamana ya kukagua Usafi. Maana kama tunakubali wenyewe kuwa uchafu ni sehemu ya maisha yetu, basi tunahitaji kubadilika tofauti na hawa unaokaribia kuwaona katika Picha inayofuata jinsi walivyotulia tena mwingine ana Pozi zuri kweli juu ya rundo la uchafu!!! Tena wengine ni wafanya Usafi lakini hawana vitendea kazi!!!



Wasukuma wana kauli fulani inasema, "mashikolo mageni." Je usafi kwetu ni kitu kigeni na hatuwezi kukitekeleza?

Tanzania bila kipindupindu na magonjwa mengine yanasababishwa na Uchafu inawezekana endapo tu kila mmoja atabadilika. Ni hayo tu.