”Egraaa, utini weeeena……” haa haa haaa. Jamani ni salamu tu hiyo ya kisauzi sauzi; ni kama ‘habari yako’ kwa Kiswahili. Mambo ya kuelekea Kombe la Dunia 2010 katika ardhi ya Madiba.
Nakualika katika ukurasa huu ikiwa leo nina ajenda ya suala zima la kukabiliana na matukio ya Moto. Mara kadhaa katika jamii zetu hizi tumekuwa tukisikia matukio mbalimbali ya Moto yakitokea, na kwa matukio hayo wapo ambao wamepata majeraha makubwa na pengine ulemavu wa maisha.
Na wapo ambao wamepoteza maisha baada ya kukumbana na mikasa mbalimbali ambayo inatokana na majanga ya Moto. Jamani moto……moto….moto…..motoooooooo!
Kikubwa kinachoonekana baada ya majanga hayo kutokea ni changamoto ya kuukabili moto. Namaanisha kuwa wengi wetu bado hatujawa na uelewa ama mbinu za kupambana na majanga hayo…..matokeo yake huwa tunachanganyikiwa mapema na kushindwa pa kuanzia pindi tu moto unapowaka.
Tumewahi shuhudia pia matukio hayo yakisababisha watu kupoteza mali zao nyingi sana; wapo ambao wameangukia katika umasikini na mifano halisi ni maeneo ya biashara mathalani soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya pamoja na jengo la ushirika jijini Dar es Salaam ambapo majanga hayo yamewafanya wafanyabiashara kuwa masikini.
Historia ya Majanga ya Moto inaziangukia pia Shule mbalimbali za hapa nchini hususani Shule za Bwezi za Sekondari; Miongoni mwa matukio hayo ni lile la mwaka 1994 mkoani Kilimanjaro katika shule ya Sekondari Shauritanga ambapo zaidi ya wanafunzi Arobaini walipoteza maisha. Pia mwaka 2009 mkoani Iringa katika shule ya Sekondari Idodi, zaidi ya wanafunzi Kumi walipoteza maisha huku wengine zaidi ya Ishirini wakijeruhiwa vibaya na janga la moto.
JAMANI JAMANI!!!!
Wananchi wakishuhudia Miili ya baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Idodi mkoani Iringa.
INAUMA!
Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi Mheshimiwa Mwantumu Mahiza akilia kwa uchungu baada ya kushudia Mabinti wa Idodi waliteketea kwa janga la Moto.
Mungu azilaze roho za marehemu wote waliopoteza maisha kwa vifo vya namna hiyo ambavyo naamini ni kati ya vifo vya mateso sana katika dunia hii. Inauma.
Hivi karibuni jijini Mwanza, Kikosi cha Zimamoto na uokoaji cha jijini humo kimeanza mkakati mwingine wa utoaji mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto kwa wanafunzi wa Shule za msingi na Sekondari.
Bila shaka huu ni mpango mbadala na kwa kweli ni tofauti na ilivyozoeleka hapo awali kwa vikosi hivyo hapa nchini kutoa mafunzo ya namna hiyo kwenye viwanda, mashirika ya umma na binafsi pamoja na karakana mbalimbali…..lakini safari hii wamehamia kwa wanafunzi.
TWENDE KAZI SASA....MAFUNZO KWA VITENDO!!!!
Afisa wa Zimamoto jijini Mwanza Bwana Masood Gadafi akiwasha moto ikiwa ni ishara ya kuanza mafunzo.
Kwa kuzingatia msemo wa Wahenga wa Kale kwamba “Mtoto mkunje angali mbichi,” mafunzo hayo yamewalenga zaidi Wanafunzi lakini pia Walimu wao hawakuwekwa kando. Na lengo kuu hapa ni kuhakikisha kuwa watu wanakuwa na ujasiri wa kuwahi kuuzima moto mapema kabla haujasambaa.
Mbinu ya kwanza ni kuuzima moto kwa kutumia Blanketi maalumu (sasa kama hauna hilo Blanketi maalumu inakuaje?)
MWENDO WA KINYONGA NA UOGA JUU!!!!
Mwalimu Patrick Leonidas wa Shule ya Msingi Igoma akiwa na Blanketi maalumu tayari kuukabili moto unaoanza kuwaka.
Sasa Wataalamu wa Zimamoto wanasema kuwa kama hauna Blanketi hilo maalumu, unachofanya ni kutumia Blanketi lako la kawaida la kujifunika wakati wa baridi au unatafuta nguo ambayo unaamini ni kati ya nguo nzito ulizonazo….halafu hiyo nguo nzito ama Blanketi unalilowesha na Maji mengi kisha unaweza kuuzima Moto huo kabla haujasambaa.
“Heeeeeee Mwalimu wetu muogaaaaaa!”
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Igoma wakimshangilia Mwalimu wao Fatuma Mrumbi wakati akiukabili Moto.
Wataalamu wanasema ukishaweza kuubeba ujasiri wa kuufunika Moto huo kwa Blanketi, basi unakuwa umeweza kuepusha ile hali ya hewa kusambaa na kuufanya moto huo kuleta madhara na uharibifu mkubwa.
Mbinu nyingine ni ya kuzima Moto kwa kutumia gesi. Na mbinu zote hizo mbili ni lazima mzimaji akae upande ambao upepo unatoka.
Wanafunzi na Walimu wa Shule ya Msingi Igoma jijini Mwanza wakifuatilia kwa makini zoezi la kukabiliana na Moto unaoanza kuwaka.
Fikra zangu zinanishawishi kuamini kuwa Kikosi cha Zimamoto na uokoaji jijini Mwanza kimepiga hatua kwa kufikiria na kuamua kufikisha elimu hiyo kwa Wanafunzi wa shule ya msingi. Wanasaikolojia wanaamini kuwa Watoto wana uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo.
Kwa mujibu wa Bwana Julius Bulambu ambaye ni Mkuu wa kikosi hicho jijini Mwanza, wamechukua hatua hiyo kutokana na uzoefu walioupata kutoka katika baadhi ya nchi zilizoendelea kama vile Finland ambayo imepiga hatua ya kupambana na majanga ya moto kwa kufikisha mafunzo ya namna hiyo mara kwa mara kwa Wanafunzi.
Pengine kitu kingine cha msingi nachokiona ni kuwa shabaha ya kuwalenga watoto inaweza kuleta mabadiliko katika jamii…..na pengine taifa hilo la leo linaweza kuwa chachu nzuri ya kueneza elimu hiyo kwa jamii kulingana na walichojifunza.
Na endapo Wizara ya Elimu italiona hili, basi itakuwa ni vyema na kupendeza ikiwa Wizara hiyo itafikiria kuifanya elimu ya majanga ya moto kuwa ni sehemu ya mtaala katika masomo ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari hapa nchini.
Ninathubutu kuyanena hayo kwa kuwa ninaona wazi mpango huo utaisaidia jamii kupambana na Moto katika hatua za awali kabla ya Zimamoto hawajafika katika eneo la tukio. Sio kila siku tukae tunawasubiri kwa muda mreeefu wafike ili hali tukijua wazi kuwa Kikosi hicho bado hakijawa na uwezo wa kutosha.
Kazi kwenu na kila la kheri Zimamoto jijini Mwanza katika mpango wenu kufikisha elimu hiyo kwenye mikusanyiko ya watu wengi kama vile kwenye masoko na vituo vikuu vya usafirishaji wa abiria.
Wabilah Tawfiq. Aslaaam Aleikum.
No comments:
Post a Comment