Je unakumbuka?Mwaka 2005 wakati Rais Ja kaya Mrisho Kikwete akijinadi kwa Watanzania ili aweze kupata nafasi aliyonayo sasa, aliwaahidi Wabongo kuwa ataongeza ajira kwa vijana......vijana hawa unaowajua ambao kwa asilimia kubwa wanalijaza Taifa.
Hoja ni je, ahadi ya Mheshimiwa JK inatekelezeka? Wakati baadhi yetu tukiendelea kuwa na Swali kama hilo vichwani mwetu, baadhi ya wakosoaji wa ahadi hiyo wanasema kuwa hali imeonekana kuwa bado si nzuri kutokana na vijana wengi kukosa ajira. Na Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2009 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mamilioni ya vijana nchini wameendelea kukosa kazi ama ajira rasmi.
"NASAKA BIDHAA LAKINI SOKO JE.....!!!!!
Baadhi ya Vijana hawapo nyuma katika utafutaji na kila kukicha wanasaka shughuli mbalimbali za uzalishaji ili waweze kujikimu na maisha yao. Kijana kama huyo hapo juu angalau ana mahali pa kuingizia riziki lakini uhakika wa soko la kazi yake upo vipi?
Kizazi kichanga kama hiki kinapojibiidisha kwa nguvu zote na kukosa masoko ya bibdhaa zao inamaanisha nini? Kwa mtindo huo tunawezaje kuwaaminisha kuwa shughuli zao zitawawezesha kupiga vita umasikini? Naamini Masoko ya uhakika kwa ajili ya shughuli zao itakuwa ni kichocheo maridhawa kinakachomhamasisha kijana kujishughulisha kwa bidii na kuondokana na umaskini.
Nikirejea tena katika utafiti wa LHRC, wanasema kuwa zaidi ya Watanzania milioni 2.3 kwa upande wa Tanzania Bara wanafanya kazi zisizo rasmi. Na wengi wa wafanyakazi hao ni vijana ambao wanafanya kazi ndogo ndogo maarufu kama ‘machinga.’ Dar es Salaam peke yake inakadiriwa kuwa na zaidi ya vijana milioni 1.6 ambao hawana ajira ya uhakika.
SHUBIRI YA JUA KALI LA SEKTA ZISIZO RASMI!!!!!!
Masikini Kijana kama huyo 'Machinga' wa mjini Dodoma baada ya kuzunguka sana juani bila kupata chochote, ona sasa ameuchapa Usingizi hadharani pasipo mapenzi yake. Biashara anayofanya ni ya kuuza visu. Na hapo akinogewa na usingizi tu anaviangukia visu vyake ambavyo ameviweka kwenye Meza!!!!!!
Moja ya mambo yanayotajwa kama kichocheo cha Vijana wengi kukosa ajira ni ukosefu wa mfumo mzuri wa elimu. Hali hiyo inasababisha vijana wengi kushindwa kupata ajira pindi wamalizapo shule kutokana na kukosa elimu ya vitendo kwani nadharia imechukua nafasi kubwa mashuleni ikiwa hali hiyo haiendani na kabisa na mazingira halisi ya ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia.
FANYA KAZI KAMA MTUMWA HATA KAMA HAZINA MALENGO!!!!!!
Kijana kama huyo licha ya kuwa anawaburudisha watu wengi hapo ambao wanamtazama, kwa mtazamao wangu siwezi kuamini kuwa anafanya kazi yenye malengo kwa maisha yake ya baadae. Jasho linamtiririka kweli lakini mwisho wa siku anabaki na nini cha kumnufaisha zaidi ya kupewa sifa za kijinga tu kuwa "haaaaaa! Yule Mshikaji anakata mauno!!!!!!"
Sina mengi ya kusema. Mara nyingine napata wasiwasi kuwa hata sauti yangu itakauka wakati sina uhakika kama wawakilishi wa vijana huko Serikalini wanafikwa na maneno ama manunguniko kama haya! Lakini kwa kuwa ni muhimu kusema na nina uhuru wa kuelezea hisia zangu, basi.........
Serikali iendelee kuweka nguvu zaidi kwenye kuongeza ajira kwa vijana wenye sifa ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza kitaaluma ili waweze kutoa mchango mkubwa kwa taifa lao ambalo linawategemea kwani wao ndio nguvu kazi. Uwekezaji 'unaowezekana' kama wa kutengeneza dawa za kienyeji, ukulima wa matunda na nyingine nyingi waachiwe vijana na wazawa. Vijana waelimishwe juu ya mambo yanayowahusu kama vile kujua sera za maendeleo zinazowahusu wao.
VIJANA SI TAIFA LA KESHO. VIJANA NI TAIFA LA LEO.
No comments:
Post a Comment