Monday, May 3, 2010

"ELIMU YA USAFI MASHIKOLO MAGENI?"

U bukheri jamani Msomaji wangu wa Ukurasa huu? Habari za siku nyingi. Mimi nafurahi na ninaona jinsi gani ilivyo vyema na kupendeza ambapo Mimi na Wewe tunakutana tena, tunakaa pamoja kwa umoja kuelezana mambo kadha wa kadha.

Jamani mara nyingi tumekuwa tukisikia harakati mbalimbali za kupambana na magonjwa ya milipuko mathalani Kipindupindu ambacho kila Mwaka kinakuja, watu wanalazwa kwa sana tu, wengine wanapoteza maisha; na kwa kuwa ni Ugonjwa wa msimu, basi inafikia hatua unatoweka na maisha yanaendelea kama kawaida.

Wapo wanaowanyooshea vidole Maafisa ama Mabwana na Mabibi afya wetu kuwa wanazembea sana katika suala la kuhamasisha Usafi. Kwa namna fulani ukweli inawezekana upo hapo; wala sibishani na huo mtazamo.

Tuuangalie upande wa pili. Hapa najitazama Mimi binafsi; jitazame na Wewe tukiwa wadau muhimu wa suala la Usafi. Nakualika hapa......



Hivi hao jamaa wote hawajui umuhimu wa kuwa wasafi? Hawajui umuhimu wa kuishi kwenye Mazingira ya usafi? Hawajui kuwa eneo kama hilo ni hatari kwa afya zao? Kisingizio cha ukata wa maisha kinaweza kuwa sababu ya kukubaliana na hiyo Picha?

Ninachotaka kusema ni kuwa.....Usafi ni suala la Mtu binafsi; wala haliitaji nguvu kutoka kwa Mtu mwingine eti aje akuhamasishe uwe msafi. Tuchukue tu mfano mdogo wa maisha yetu ya kila siku. Jiulize ni mara ngapi unanawa Mikono yako punde tu unapotoka Chooni!! Haijalishi umetoka kupata haja ndogo ama kubwa!!!????

Kwa mtindo huo wala hatuitaji kuwalaumu hao wenye dhamana ya kukagua Usafi. Maana kama tunakubali wenyewe kuwa uchafu ni sehemu ya maisha yetu, basi tunahitaji kubadilika tofauti na hawa unaokaribia kuwaona katika Picha inayofuata jinsi walivyotulia tena mwingine ana Pozi zuri kweli juu ya rundo la uchafu!!! Tena wengine ni wafanya Usafi lakini hawana vitendea kazi!!!



Wasukuma wana kauli fulani inasema, "mashikolo mageni." Je usafi kwetu ni kitu kigeni na hatuwezi kukitekeleza?

Tanzania bila kipindupindu na magonjwa mengine yanasababishwa na Uchafu inawezekana endapo tu kila mmoja atabadilika. Ni hayo tu.

No comments:

Post a Comment