Mwaka huu Bunge letu la Jamhuri ya muungano wa Tanzania liliifanyia marekebisho Sheria ya Usafirishaji na hatimaye Pikipiki na Baiskeli zimeruhusiwa kupakia Abiria kibiashara kwa kutoza Nauli.
Lakini kwa upande wa Pikipiki, utaratibu huu una masharti yake. Dereva wa Pikipiki anatakiwa kuzifahamu sheria za barabarani ikiwemo na kuwa na leseni. Dereva na Abiria wa Pikipiki wanatakiwa kuvaa Kofia maalumu kichwani a.k.a HELMET.
Aina hii ya usafiri wa abiria kwa kutumia Pikipiki a.k.a BODABODA kwa baadhi ya maeneo kama unavyojulikana hususani kanda ya ziwa, umeanza kuwa maarufu sana kwa sababu ni wa haraka na isitoshe bei ni nafuu ukilinganisha na usafiri mwingine wa haraka mathalani Taksi.
Tatizo sasa ni kutokufuatwa kwa sheria za barabarani huku Madereva wengi wao wakiwa ni vijana kusemekana kuwa wanaendesha hovyo huku utafiti wa kipolisi ukisema kuwa wengi wao huwa wanaingia barabarani wakiwa wamefyonza viroba!
Cha ajabu kingine ni kwamba si jambo la ajabu sana kukuta aidha Dereva amevaa HELMET huku abiria akiwa hana au kibaya zaidi kukuta wote (Dereva na Abiria) hawana hiyo HELMET.
Mpya kuliko zote sasa. Kuna tabia ya kupakia Abiria zaidi ya mmoja. Unakuta Dereva wa Pikipiki kapakia Abiria Wawili au zaidi katika Pikipiki moja! Mtindo huo wa upakiaji kwa huku Mwanza unajulikana kama MSHIKAKI!
Lakini hata sheria hiyo iliyobarikiwa na Bunge inasisitiza matumizi sahihi ya Pikipiki likiwemo hilo la kupakia Abiria mmoja tu katika Pikipiki.
Hawa Madereva ni viburi kwa kisingiziio kuwa Bunge limeubariki usafiri huo. Inastaajabisha kuwa Pikipiki hiyo iliyopakia Abiria zaidi ya mmoja inakatiza mbele ya Macho ya Askari wa barabarani na wala hakuna hatua zinazochukuliwa.
Kutokana na uzembe huo pamoja na mengine niliyoyataja hapo juu ndani ya usafiri huu wa Pikipiki, baadhi ya mikoa imeshuhudia kuongezeka kwa ajali za usafiri wa Pikipiki. Watu wanakufa. Watu wanapata majeraha ya kudumu.
Mikoa mingine katika hospitali zao za mikoa na nyingine za rufaa imefikia hatua ya kutenga wodi maalumu za majeruhi wa pikipiki!
Tunakwenda wapi? Tunawafanya nini hawa Madereva Pikipipiki. Tunaudhibiti usafiri huu ili usiendelee kugharimu maisha ya Watanzania?
No comments:
Post a Comment