Saturday, June 26, 2010

KUMEKUCHAAAA......


Moja ya vitu ambavyo huwa napenda kuviona katika Dunia hii ni pale Jua linapokuwa linachomoza! Huwa napenda sana hiyo mandhari na wakati mwingine huwa inanifanya nitulie kuangalia hilo tukio zima, wakati huo huo napata nafasi nzuri ya kutafakari mambo mbalimbali.

KOMBE LA DUNIA


Hizo Antena zimenyooka kwa wingi sana katika paa za nyumba za Uswazi. Kombe la Dunia hapo linaonekana live bila chenga. Waswahili watundu sana jamani. Yaani TUBE LIGHT kuwa Antena!!!!!?????

Friday, June 11, 2010

HIFADHI YA SERENGETI YAONGEZWA UTAJIRI

Serengeti ni kati ya hifadhi za Taifa ambazo zinawavutia watalii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Ni hifadhi ambayo ukipata nafasi ya kuitembea, basi nafsi yako itafurahi kwa kuona Wanyama weeeengi…


Swala wanaonekana kwa wingi sana…


Nyumbu nao vilevile…


Viboko wazee wa majini…


Hata Nyani nao wamo…


Hao ni baadhi tu. Lakini pia katika hifadhi hiyo, wapo Twiga, Pofu, Tembo, Chui, Mbuni, Pundamilia na wengine kedekede! Na hivi karibuni Hifadhi hiyo imeongezwa thamani……imeongezwa utajiri.

Mwezi wa Tano 2010, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitua katika hifadhi hiyo…


Vikundi mbalimbali vya utamaduni wa Mtanzania vikamkaribisha yeye na wageni alioongozana nao siku hiyo…




Mengine hayakumstaajabisha yeye tu, bali hata aliokuwa nao pia walibaki duuuuuuuuu!


Umeshawahi kuona Viatu kama hivyo hapo! Katika mazingira ya kawaida lazima uvishangae……


Ni kati tu ya burudani za asili ya Mtanzania ambazo zilionyweshwa siku hiyo katika hifadhi ya Serengeti.

Si Rais Kikwete tu…..vyombo mbalimbali vya habari vilifunga safari mpaka kwenye hifadhi hiyo kushuhudia utajiri huo ambao umeongezwa Serengeti.

Waandishi kutoka nchini walikuwepo…


Wengine walitoka SABC (Afrika Kusini), AP, REUTERS na kwingineko…




Na hata Balozi wa Marekani nchini Bwana Alfonso alikuwepo kufuatilia tukio hilo. Ona sasa alivyokuwa amejiachia……


Jamani wote hao walikusanywa na tukio moja tu. Ni la kurejeshwa kwa Faru weusi watano kati ya 32 ambao wanaingia nchini wakitokea huko Afrika Kusini. Historia inasema Faru hao wana asili ya Afrika Mashariki.

Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Faru hao walipungua nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla kutokana na vitendo vya ujangiri. Wapo waliokuwa wanawawinda wanyama hao eti kwa kuwa Pembe zao zikisagwa zinatoa unga ambao ni dawa nzuri ya kuongeza nguvu za kiume!

Hali hiyo ilipelekea kuchukuliwa kwa Faru wachache waliokuwepo, kisha wakapelekwa Afrika Kusini……..wakahifadhiwa na wakazaliana huko…….na hatimaye baada ya miaka takribani 50 kizazi cha Faru hao kimerejea nchini……


Ndege ikatua salama katika ardhi ya Tanzania, kisha ikafunguliwa……


Faru hao inasemekana hawatachukua muda mrefu kuyazoea mazingira yao ya awali pamoja na vyakula vinavyopatikana Serengeti. Na kwa kuanzia wameletwa na vyakula vyao vya muda……


Hatimaye wakaanza kushushwa…


Ilikuwa ni vigumu kuwaona kwa kuwa walikuwa katika makasha maalum…..na ulinzi ulianza kuimarishwa hapo hapo katika kiwanja kidogo cha ndege cha Seronera…


Kisha wakapakizwa kwenye Magari……
kvumjnh


Na safari ya kuelekea katika hifadhi ya Serengeti ikaanza…..


Hapo awali nimesema hifadhi ya Serengeti ina wanyama wengi lakini kwa sasa imeongezwa utajiri. Sababu ni kuwa Faru ni kati ya Wanyama watano wanaopendwa sana na Watalii duniani.

Sababu ya ujangiri haiitishi tena Serikali kwani Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Shamsa Mwangunga anasema kuwa kwa sasa wamejipanga kutokana na mafunzo mbalimbali ambayo wamekuwa wanawapatia Askari wao.

Wananchi nao wanasema ushirikiano wa kuwalinda wanyama pori kwa sasa upo kwani angalau wananufaika na kuwepo kwa rasilimali hizo. Wanasema siku hizi wanaona sehemu ya mapato yanayopatikana yanatumika kuimarisha miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Nae Rais Kikwete anasema dhana ya ulinzi hisiwape tena hofu Watanzania. Kwa nini? Anasema Faru hao watakuwa wanalindwa kwa Saa 24! Na kikubwa zaidi watakuwa na ulinzi wa kipekee kama wanavyolindwa viongozi wa nchi. Kila Faru atakuwa na mlinzi wake katika hizo Saa 24.


Kufikia mwaka 2013/2014 Serikali inatarajia kuwa Faru hao 32 wanaokuja kwa mafungu mafungu, watakuwa wameingia nchini na kusambazwa katika hifadhi mbalimbali za Taifa.

Kazi kwetu Watanzania kuushabikia utalii wa ndani.